James 1

1Yakobo, mtumwa wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, kwa makabila kumi na mbili yaliyotawanyika, salaam. 2Hesabuni kuwa ni furaha zaidi, ndugu zangu, mnapopita katika matatizo mbali mbali, 3mkijua kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huwapa uvumilivu.

4Acheni uvumilivu uikamilishe kazi yake, kwamba muweze kukomaa kikamilifu, bila kupungukiwa katika lolote. 5Lakini kama mtu kati yenu anahitaji hekima, aiombe kutoka kwa Mungu, ambaye hutoa kwa ukarimu na pasipo kukemea kwa wote wamwombao, na atawapa hekima.

6Lakini omba kwa imani, bila shaka, kwa kuwa mwenye kutia shaka ni kama mawimbi katika bahari, huchukuliwa na upepo na kutupwa huku na huko. 7Kwa hakika mtu huyu asifikirie kwamba atapokelewa ombi lake kutoka kwa Bwana; 8mtu huyu ana nia mbili, si imara katika njia zake zote.

9Ndugu maskini anapaswa kujivuna katika kusimama kwake juu, 10wakati huo huo ndugu tajiri katika unyenyekevu wake, kwa sababu atatoweka kama ua la kondeni katika shamba analopita. 11Jua huchomoza na joto la kuunguza kukausha mimea, na maua huanguka na uzuri wake hufa. Vivyo hivyo watu matajiri watachakaa katikati ya kazi zao.

12Amebarikiwa mtu yule anayevumilia majaribu, kwa kuwa baada ya kushinda jaribu hilo, atapokea taji ya uzima, ambayo imeahidiwa kwa wale wampendao Mungu. 13Mtu yeyote hapaswi kusema anapojaribiwa, “Jaribu hili linatoka kwa Mungu,” kwa sababu Mungu hajaribiwi na uovu, na Mungu mwenyewe hamjaribu yeyote.

14Kila mtu hujaribiwa na tamaa zake mbaya zinazomshawishi na kumvuta mbali. 15Ndipo baada ya tamaa ya dhambi kubeba mimba, dhambi huzaliwa, na baada ya dhambi kukomaa sawasawa, huishia katika mauti. 16Ndugu zangu wapendwa, msidanganyike.

17Kila zawadi iliyo nzuri na kila zawadi iliyokamilika hutoka juu, hushuka chini kutoka kwa Baba wa nuru. Kamwe habadiliki kama kivuli kibadilikavyo. 18Mungu alichagua kutupa sisi uzima kwa Neno la kweli, ili kwamba tuweze kuwa kama uzao wa kwanza miongoni mwa viumbe vyake.

19Mnajua hili, ndugu zangu wapendwa. Kila mmoja anapaswa kuwa mwepesi wa kusikia, siyo mwepesi wa kuongea wala kukasirika, 20kwa kuwa hasira ya mwanadamu haiwezi kutenda haki ya Mungu. 21Kwa hiyo wekeni mbali uchafu wa dhambi na ubaya wote ulio mahali popote, na kwa unyenyekevu lipokeeni neno lililopandwa ndani yenu, ambalo lina uwezo wa kuokoa roho zenu.

22Litiini neno, msilisikie tu, mkijidanganya nafsi zenu wenyewe. 23Kwa kuwa kama yeyote alisikiaye neno bila kulitendea kazi ni sawa na mtu ajiangaliaye uso wake halisi katika kioo. 24Hujitathimini uso wake, na huenda zake na baada ya muda mfupi husahau anavyofanana. 25Bali mtu yule anayeiangalia kwa uangalifu sheria kamili, sheria ya uhuru, na kuendelea kuitii, si kwa sababu yeye ni msikilizaji anayesahau, huyu mtu atabarikiwa anapoitenda.

26Ikiwa mtu yeyote atafikiri mwenyewe kuwa ni mtu wa dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, huudanganya moyo wake na dini yake ni bure. Dini iliyo safi na isiyoharibiwa mbele za Mungu wetu na Baba ni hii: kuwasaidia yatima na wajane katika mateso yao, na kujilinda wenyewe na ufisadi wa dunia.

27

Copyright information for SwaULB